JE, TUKIWASHUGHULIKIA WATUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA TUWAACHE MAJAMBAZI PATA HABARI HAPA.

Mihadarati sawa; tusiwasahau majambazi, matapeli viwanja

“SISI tumekwisha uwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu ulete tumaini pale ambapo hapana matumaini, upendo penye chuki na heshima ambapo pamejaa dharau.”
Maudhui ya wimbo huu ulioimbwa siku Tanzania ilipouwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro yameanza kuonekana katika Tanzania mpya tnayoiona sasa. Serikali “imewasha mwenge” wa vita dhidi ya dawa za kulevya kwa wazalishaji, wasafirishaji, wauzaji na watumiaji.
Vita hii inahitaji nguvu ya pamoja kwa kuwa madhara ya dawa za kulevya yanawakumba wana jamii wote kiuchumi, kijamii na kiafya. Hii iwe vita ya wote. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inaonekana kuthubutu kuutafuna mfupa uliowashinda wengi.
Rais Magufuli ameridhia, amebariki na kuagiza vita ianze na kuendelea bila mwisho. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tayari “wamewasha moto” na katika hatua za awali, mafanikio makubwa yanaonekana na kuanza kurejesha matumaini kwa Watanzania.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rodgers Sianga, Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka hiyo, Mihayo Msikela na Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka, Fredrick Kibuta, wamesema vita hii haitamwacha yeyote aliyejihusisha na mihadarati wala mali iliyochumwa kutokana na mihadarati haitabaki nyuma ya sheria. Orodha iliyotolewa ya watuhumiwa wa kujihusisha na dawa hizo inaonesha kuwa Serikali imenuia kupambana kuwanusuru na kuwaokoa Watanzania.
Safari hii, wanaotajwa si tu “dagaa” ambao ni wagonjwa walioathirika na dawa hizo, bali pia vigogo na mapapa wanaofikishwa mbele ya sheria ili haki itendeke. Vita hii ni kubwa na hatari na ndiyo maana Rais Magufuli na Makonda wanawaomba Watanzania na viongozi wa dini, wawaombee.
Kwa pamoja, tutashinda kwa kishindo. Wakati vita hii katika hatua za awali inaonesha mafanikio na ushindi, tusiisahau vita dhidi ya ujambazi, wizi na uhalifu wa kutumia silaha ambao umeangamiza maisha na mali za Watanzania wengi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na makamanda wa mikoa mingine ikiwamo ya Tanga, Mbeya, Mwanza na mikoa mingine, mara nyingi wanalia na kukosa mapumziko kutokana na ujambazi unafanywa kwa kupora na kuua Watanzania wakiwamo baadhi ya askari kuuawa.
Ufike wakati sasa majambazi nao wachunguzwe na kutakiwa kuripoti polisi haraka kama wanavyofanywa “wazungu wa unga” na waathirika ili nao wachunguzwe; muda wa kubembeleza uhalifu sasa uishe ili Tanzania niwe mahali pema pa kuishi kwa watu wote.
Waitwe hadharani hata matapeli wa haki za wengine wakiwamo matapeli wa viwanja wanaowadhulumu wanyonge wakiwamo wajane na yatima wakishirikiana na baadhi ya watumishi wasio waadilifu katika idara za ardhi.
Hao, ni wale wanaotumia ubabe wa fedha na mabaunsa kupora haki za wanyonge. Wapo wengine wanaojificha kwenye mwavuli wa dini, lakini matendo yao hao siyo ya kidini, bali ni “makupe” wanaoishi kwa kunywa damu ya Watanzania wanyonge.
Hao, wachunguzwe kwa nini wengine wanajificha katika kulazimisha urafiki na baadhi ya viongozi wa dini na serikali waadilifu ili kujificha chini ya kivuli chao bila wahusika kujua. Hao, kwa Tanzania mpya, wasipone.
Wachunguzwe kama kazi wanazofanya na maisha wanayoishi vinawiana. Wachunguzwe hata biashara na huduma zao zinalipa kodi ipasavyo kuchangia pato la taifa.
Wachunguzwe hata misaada, misamaha ya huduma wanazopewa kama inatumika kwa malengo. Mfano, viwanja vya kujenga vituo maalumu kusaidia wanyonge, kama kweli vinafanya kazi hiyo, au wanaidanganya Serikali kisha kuuza viwanja na huduma hizo huku wengine wakiwa na miradi ya kuajiri watu na kuwaachisha bila kuwapa haki zao.
Waulizwe kama kweli wako juu ya Serikali hii tukufu, au wanaijaribu. Waulizwe wanajiamini na kujivunia nini; watajwe, waitwe, wahojiwe na wafikishwe mbele ya sheria. Tuitengeneze Tanzania yetu iwe mpya.

Comments

Popular posts from this blog

Picha ya kutisha ya Mtoto wa miezi nane kulawitiwa na baba yake mzazi.

MAJANI YA MPERA NA FAIDA ZAKE MWILINI.